SIMBA YAANZA MAWINDO MAPEMA HUYU HAPA MWAMBA KUTUA MSIMBAZI

SIMBA YAANZA MAWINDO MAPEMA HUYU HAPA MWAMBA KUTUA MSIMBAZI

Klabu ya Simba SC imeanza harakati za kuboresha kikosi chake kuelekea msimu mpya kwa kuhusishwa na mazungumzo ya kumsajili beki wa kushoto wa Al Hilal ya Sudan, Khadim Diaw, mwenye umri wa miaka 26. Hatua hii inalenga kumuongezea nguvu na ushindani nahodha wao wa sasa, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Simba, klabu hiyo ina mpango wa kuachana na beki raia wa Burkina Faso, Valentine Nouma, ambaye ameripotiwa kuomba kuondoka baada ya kukosa nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza.

Nouma pia hakufanikiwa kumpa changamoto ya kutosha Tshabalala, ambaye licha ya kuwa na mchango mkubwa, ameonekana kuchoka kutokana na kutumika mfululizo.

“Simba ipo katika mchakato wa kuzungumza na wachezaji mbalimbali wazawa na wageni ili kuboresha timu kwa ajili ya msimu ujao,” kilidokeza chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo.

Ripoti ya kocha Faldu Davis ndiyo itakayokuwa msingi wa maamuzi ya nani atabaki na nani ataachwa kikosini. Simba imeweka malengo makubwa kwa msimu ujao, ikiwa ni pamoja na kupambana kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kufanya vyema katika michuano ya CAF Champions League.

Khadim Diaw, anayewindwa na Simba, ni mmoja wa wachezaji waandamizi wa Al Hilal ambao msimu huu walitinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Pia, alisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Mauritania licha ya kuwa timu iliyoalikwa.

Endapo usajili huu utafanyika, utakuwa ni hatua muhimu kwa Simba katika kulijenga upya safu ulinzi, huku ikilenga kuongeza ushindani wa namba na kuleta safu imara ya wachezaji watakaosaidia klabu hiyo kufikia malengo makubwa yaliyowekwa.

Add a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *