MZIZE NA DUBE JUKUMU LAO NI MOJA TU LEO

MZIZE NA DUBE JUKUMU LAO NI MOJA TU LEO
Leo macho ya mashabiki wa soka yatakuwa Mbeya, ambapo mabingwa watetezi Yanga SC watashuka dimbani kwenye Uwanja wa Sokoine kuivaa Tanzania Prisons katika mchezo wa raundi ya 29 wa Ligi Kuu ya NBC.
Huu si mchezo wa kawaida tu kwa Wananchi, bali ni fursa muhimu kwa washambuliaji wao mahiri Prince Dube na Clement Mzize kujiimarisha katika mbio za kuwania kiatu cha dhahabu cha ufungaji bora.
Yanga inahitaji ushindi ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutetea taji lao la ligi, lakini Dube na Mzize wana ajenda yao binafsi, kuongeza idadi ya mabao na kumkaribia au kumpiku mfungaji anayeongoza kwa sasa, Jean Charles Ahoua wa Simba SC, ambaye tayari amefunga mabao 15.
Kwa sasa, Dube na Mzize wako sawa kwa mabao 13 kila mmoja, tofauti ya bao mbili tu kutoka kwa Ahoua. Kwa kiwango wanachoonesha, si jambo lisilowezekana kwa mmoja wao au wote wawili kufikia na hata kuvuka idadi hiyo katika mechi tatu zilizosalia.
Mechi ya leo dhidi ya Tanzania Prisons ni muhimu sana, sio tu kwa Yanga kama timu, bali kwa wawili hao wanaotazamwa kama injini mpya ya mashambulizi ya Wananchi.
Clement Mzize, kijana anayeendelea kungβara kwa kasi, ameonesha kuwa hana woga mbele ya lango, huku Prince Dube akiwa na uzoefu mkubwa wa kutafuta mabao katika mazingira magumu. Kombinasheni yao imekuwa tishio kwa safu nyingi za ulinzi msimu huu, na leo uwanja wa Sokoine unaweza kuwa jukwaa lingine la wao kungβara.
Mechi tatu zilizosalia ni kama fainali kwa Yanga katika kutetea ubingwa lakini pia kwa Dube na Mzize katika kutengeneza historia binafsi

