ALLY MAYAY AWEKA NGUMU RAIS KARIA KUPITA BILA KUPINGWA TFF

Nyota wa zamani wa Yanga SC na Taifa Stars, Ally Mayay ametangaza rasmi nia ya kugombea Urais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti 16, 2025, jijini Tanga.

Mayay, anayejulikana kwa uzalendo wake, umahiri ndani na nje ya uwanja na ushawishi mkubwa katika mijadala ya soka kitaifa, anaingia kwenye mbio hizi akiwa na malengo ya kuleta mabadiliko makubwa kwenye uendeshaji wa mchezo huo.

Kwa muda mrefu, mashabiki na wadau wa mpira wamekuwa wakihitaji uongozi unaojali maendeleo ya mpira kuanzia ngazi za chini, na sasa Mayay anaonekana kujibu wito huo.

Licha ya kuwa kwenye kipindi kigumu cha maombolezo kufuatia kifo cha baba yake mzazi kilichotokea mkoani Tabora, leo saa 7 mchana, mwakilishi wake atachukua fomu ya kugombea kwa niaba yake, ishara ya dhamira thabiti ya kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi huo mkubwa wa kihistoria.

Hii itakuwa mara ya pili kwake kuchuana na Rais wa sasa wa TFF Wallace Karia kwani katika uchaguzi uliopita alichukua fomu lakini aliondolewa katika kinyang’anyiro kwa kigezo cha kutokuwa na cheti ya kidato cha nne licha ya kuwa Mayay ni msomi mwenye Shahada ya Uzamili ya Chuo Kikuu

Mayay si jina geni kwenye tasnia ya soka nchini. Mbali na kuichezea Yanga kwa mafanikio, amewahi kuitumikia timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kwa uzalendo mkubwa.

Baada ya kustaafu soka, amekuwa mchambuzi makini wa michezo, mtetezi wa wachezaji pia akiwa Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Tanzania

 

Add a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *